18 Februari 2015 - 12:19
 Boko Haramu waua watu 38 Nigeria

Watu 38 wameuwawa nchini Nigeria kutokana na mashambulizi mawili yanayoaminika kufanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram. Katika tukio la kwanza, bajaji moja ililipuka mkoani Borno,

Watu 38 wameuwawa nchini Nigeria kutokana na mashambulizi mawili yanayoaminika kufanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram. Katika tukio la kwanza, bajaji moja ililipuka mkoani Borno, Kaskazini Mashariki mwa nchi. Watu 36 walikufa na wengine 20 kujeruhiwa. Katika tukio la pili mtu mmoja alilipua boma la kujitoa muhanga katika mgahawa mmoja mkoani Yobe ambapo watu wawili waliuwawa. Mashambulizi hayo yanakuja wakati ambapo kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau, ameahidi kuuvuruga uchaguzi mkuu ambao tayari umesogezwa kutoka tarehe 14 Februari hadi Machi 28 mwaka huu. Katika video iliyosambazwa mtandaoni Shekau anasema uchaguzi hautafanyika, hata kama wafuasi wa Boko Haram watakufa.

Wakati huo huo Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linakutana hii leo kujadili hali ya usalama nchini Libya baada ya waasi wa Dola la Kiislamu kuua wakristo 21 nchini humo siku ya Jumapili. Wote walikuwa raia wa Misri. Waziri wa mambo ya nje wa Misri, Sameh Shoukry, yuko jijini New York ambapo atafanya mazungumzo na wajumbe wa baraza la usalama na wawakilishi wa nchi za Kiarabu. Misri imeliomba baraza la usalama liruhusu majeshi kutoka nje yaingilie kati mgogoro wa Libya ambapo makundi ya waasi wanaohasimiana yanagombea madaraka. Hata hivyo, Libya lazima ipeleke ombi rasmi kwa Umoja wa Mataifa kama inataka msaada kutoka nje na haifahamiki kama ombi hilo litapelekwa kwani kwa sasa Libya ina serikali mbili na mabunge mawili.